Monday, May 07, 2012

"Toa Kitabu Kisomwe"-Ombi toka UDI

Asasi ya Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative-UDI) imezindua Programu ya Taarifa yenye ujumbe “Toa Kitabu Kisomwe” inayohusisha kukusanya vitabu vya kiada na vya ziada kutoka wa watu mbalimbali na taasisi mbalimbali na kuvisambaza katika taasisi za elimu kwa ajili ya wanafunzi kusoma na maeneo maalumu kwa ajili ya wananchi kujisomea. Tunaomba taasisi au mwananchi yoyote mwenye kitabu chochote popote ambaye yuko tayari kukitoa ili kisomwe iwe ni cha kiada au cha ziada awasiliane UDI ili iweze kufikisha kitabu hicho kwa walengwa. “Toa kitabu kisomwe” kupitia ofisi ya UDI iliyopo Kimara Kona au wasiliana na Ubungo Development Initiative (UDI) kupitia Afisa Taarifa (0768503331 au 0715745874) au barua pepe ubungo2005@yahoo.com kutoa kitabu husika. Ukipenda unaweza kuweka saini kwenye kitabu hicho kama kumbukumbu kuwa taasisi yenu au wewe ndiye uliye “Toa kitabu Kisomwe” au unaweza pia kutueleza kitabu hicho unapendekezwa kipelekwe wapi ndani ya Manispaa ya Kinondoni ili kiweze kusomwa kwa ufanisi. Sisi mpango wetu ni kusambaza vitabu hivyo kwenye maktaba za shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa upande wa elimu ya kiada na kusambaza kwenye maktaba za jumuia, ofisi za serikali za mtaa, taasisi za kijamii na vijiwe vya kudumu kwa upande wa elimu ya ziada. Tunaamini kwamba kwenye kaya mbalimbali za Manispaa ya Kinondoni vipo vitabu makabatini au masandukuni ambavyo ama ni vya kiada vilivyoachwa baada ya walengwa wa awali kupanda ngazi moja ya elimu kutoka ile ambayo walikuwa wakisoma au ni vya ziada ambavyo tayari wahusika walishavitumia na vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa walengwa wengine wenye kuvihitaji hivyo; “Toa Kitabu Kisomwe”. Aidha, tunaamini pia kwamba Jiji la Dar es salaam lina makao makuu ya taasisi mbalimbali ambazo hutoa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kusambaza nchini lakini wakati mwingine hushindwa kuwafikia walengwa katika ngazi ya chini jijini hivyo UDI kwa kuwa taasisi ya ngazi ya chini inaweza kuwa kiungo kizuri cha kuwezesha vitabu husika kuwafikia walengwa; “Toa Kitabu Kisomwe”.