Thursday, January 17, 2008

Barua ya wakazi wa Kibamba

WAATHIRIKA WA UHAMISHWAJI KIMABAVU LUGURUNI NA KIBAMBA HOSPITALI (WUKILUKI).
wukiluki.kibamba@yahoo.com

03 Januari, 2008
Waziri
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi

Katibu Mkuu
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi

Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Dar es Salaam

Mkuu wa Wilaya
Wilaya ya Kinondoni

Mkurugenzi
Manispaa ya Kinondoni

Yah: KUOMBA MENEJA WA MRADI WA UJENZI WA MIUNDO MBINU LUGURUNI NA KIBAMBA HOSPITALI AWAJIBISHWE KUTOKANA NA KUKITHIRI KWA VITENDO VYA RUSHWA, MALIPO YA FIDIA HEWA, BAADHI YA WATU KUZIDISHIWA KIWANGO CHA MALIPO YA FIDIA ISIVYO HALALI NA MENEJA WA MRADI KUWATISHA WATU WATOA HABARI JUU YA VITENDO HIVYO VICHAFU.

Rejea katika mazungumzo kati ya mwakilishi wa waathrika wa mardi huu na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, yaliyofanyika siku ya Ijumaa tarehe 21 Desemba 2007, yakihusu madai ya kuwepo malipo ya fidia hewa na watu kuzidishiwa malipo ya fidia isivyostahili.

Kwa mujibu wa majibu ya Kaimu Katibu Mkuu kwa mwakilishi wa waathrika baada ya kikao cha uchunguzi kuitishwa, Kaimu Katibu Mkuu alinukuliwa akisema kuwa wizara itasimamisha malipo kwa majina yaliyowasilishwa wizarani yakidaiwa kuwa ni malipo hewa. Pia Kaimu Katibu Mkuu alinukuliwa akisema kuwa imeamuliwa kuwa uhakiki wa malipo ya fidia katika mradi huu utafanyika mara moja.

Sisi waathrika tunapenda kuipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kwa kuchukua hatua za haraka ili kuokoa fedha za serikali zisipotee. Kasi hiyo ya ajabu imeijengea heshima kubwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi pamoja na viongozi wake.

Kutokana na uamuzi huo wa wizara, matendo yafuatayo yalifuatia yenye lengo la kukwamisha azma ya wizara kuokoa fedha za serikali, kuwatambua na kuwanasa wote waliolipwa fidia isvyo halali. Vitendo hivyo ni pamoja na:-

1) Waliohusika kulipwa malipo hewa kuonekana kushughulika kutafuta ardhi na majengo ya kuonyesha wakati wa zoezi la uhakiki. Hii ikashiria ya kuwa tayari wafanya uhakiki (wale wale waliohusika) wamearifiwa kufanya hivyo ili kuficha uovu.

2) Uongozi na watendaji wa mradi kuonekana mara kwa mara eneo la mradi wakati wa sikukuu za krismai na mwaka mpya wakizunguka zunguka na wanaodaiwa kulipwa malipo hewa na wanaodaiwa kuzidishiwa malipo isivyo halali.

3) Meneja wa mradi kuwapigia simu na kuwatishia Ndg Selestine Michael na Mama Edgar walionekana wakitoa malalmiko yao katika kituo cha ITV kuwa watabomolewa pasipo kulipwa fidia yoyote. Vitisho hivi vilikuwa na ari wa wananchi kutoa taarifa zaidi za vitendi viovu.

Kwa mujibu wa vitendo vilivyofuatia uamuzi huo wa serikali, sisi waathrika tuna kila sababu ya kuamini kuwa vitendo vya rushwa, malipo ya fidia hewa na baadhi watu kuzidishiwa malipo isivyo halali vilifanyika kwa ufahamu na baraka za uongozi wa mradi huu (Meneja), na ndio maana baada ya wizara kuagiza uhakiki ufanyike vitendo vya kupoteza ushahidi na kujaribu kuwanyamazisha watoa habari vinafanyika.

Tunalazimika kusema hivyo kwa kuwa meneja huyu aliwaruhusu maafisa ardhi na maafisa wa kutathmini mali (Valuers) walio chini yake kuwatumia madalali wa viwanja na nyumba katika kutambua maeneo na kuthibitisha wamiliki halali badala ya kutumia Ofisi ya serikali za Mitaa. Kutumika kwa madalali badala ya ofisi ya serikali ya kulifanyika kwa nia ya kufanikisha malipo hewa kwa kuwa dalali huyu anatambua mashamba na viwanja ambavyo wamiliki aidha wamefariki, kuwa nje ya nchi au kukaa muda mrefu pasipo kuhudumiwa.

Maafisa ardhi na maafisa wa kutathmini thamani ya mali waliokuwa chini ya meneja huyu walimtumia sana dalali wa viwanja aitwaye Ndugu Norbert Mtewele (Mbenna) kinyume na sheria za ardhi. Dalali huyu ni mjumbe wa shina eneo la Kibamba hospitali lakini aliweza kutumika na watekelezaji wa mradi huu hadi maeneo ya Luguruni, Msakuzi na Kibamba CCM na katika Mitaa ya Kwembe na Kiruvia kutambua maeneo na kuthibitisha uhalali wa wamiliki badala ta ofisi za serikali ya Mitaa husika.

Kama ujira wa dalali huyu, maafisa ardhi na maafisa wa kutathmini thamani ya mali wa mradi huu walimpatia dalali Morbert Mtewele malipo ya fidia katika jengo lililopo katika barabara ya zamani ya Morogoro, wafanyabiashara wengine zaidi ya 30 katika eneo hilo hilo walinyimwa fidia hiyo kwa kuwa barabarani. Aidha inadaiwa kuwa dalali huyu alipatiwa fidia inayozidi thamani ya jengo husika kwa zaidi ya mara 10.Vile vile inadaiwa kuwa watekelezaji wa mradi huu walitumia majina ya wadogo wawili wa dalali huyu wajulikanao (majina tunayahifadhi) kujipatia fidia isiyostahili kwa kutumia viwanja na majengo wasiyo kuwa wamiliki halali. Inakadiriwa kuwa kisai cha zaidi ya shilinngi million 40 za serikali zinazotosha kujenga madarasa 5 (tano) zimepotea kwa watu hawa watatu tu.

Sisi waathrika wa mradi huu tanaamini kwa dhati ya kuwa azma ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ya kuokoa fedha za serikali na kuwatambua watu waliolipwa isivyo halali haitafanikiwa kutokana na kukiukwa kwa “Natural Justice” katika zoezi zima la uhakiki wa malipo ya fidia ndani ya mardi huu. Haiwezekani mtendaji aruhusu/afanikishe/afanye malipo hewa halafu ajihakiki mwenyewe. Pia azma hiyo haitatekelezeka kwa kufanya uhakiki wa zima moto kwa watu waliotyajwa tuu.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa kamati yetu orodha ya watu waliohusika kulipwa malipo hewa na watu kulipwa zaidi kuliko wanavyostahili ni ndefu na itahusisha kiwango kikubwa sana cha fedha za serikali kupotea. Upo ushahidi unaoonyesha ya kuwa wapo watu ambao hawakuwa wakazi wa Kibamba kabisa ambao wamelipwa fidia na kutokomea na fedha za serikali isivyo halali. Na hii itathibitika tu pale uhakiki kamili utakapo fanyika na kuwabainisha wazi wazi kwa kuwa hadi sasa hakuna muathirika hata mmoja ambaye ameweza kuhama. Orodha iliyowasilishwa wizarani, ni ya watu wachache tu walioanza kutajwa tajwa na wananchi kuwa walihusika na vitendo hivyo.

Hivyo basi ili azma ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi ya kuokoa fedha za seriakli itimie, ipo haja ya wananchi kujengewa mazingira muafaka ya kuendelea kuwataja wahusika wote waliohusika na kulipwa fidia isivyostahili, wakiwemo maafisa ardhi waliohusika kuomba rushwa ili waweze kuwasaidia wananchi watakaokumbwa na mradi huu waendelee kubaki walipo bila ya kuhamishwa. Pia maafisa tathmini mali (Valuers) waliokuwa wakiomba rushwa ili waweze kuwaongezea watu malipo ya fidia kuliko wanavyostahili na wale waliohusika kufanikisha malipo ya fidia hewa.

Ili kuweza kujenga mazingira muafaka ya wananchi na waathrika kuwa na ujasiri wa kuwataja wote waliohusika na vitendo hivyo, ipo haja kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za makusudi zitakazo onyesha wazi wazi kuwa uongozi wa taasisi unataka kupambana na vitendo vya namna hii katika mradi huu na miradi mingine yote ya namna hii itakayofuata. Kwa kuwa hata mtukufu Rais jakaya M kkwete alishaonyesha wazi wazi kukerwa na kukuthiri kwa rushwa miongoni mwa watendaji wa masuala ya rdhi hapa nchini. Sisi waathrika tunapendekeza kuwa uhakiki wa malipo ya fidia ufanywe na watu tofauti na wale ambao wakihusika katika kujenga mazingira ya kufanikisha malipo hewa ya fidia n.k. Vile vile tunaomba wale wote waliohusika na kutowajibika ipasavyo hadi vitendo hivi vikatokea wawajibike mara moja ma wasihusike katika uhakiki wa malipo ya fidia ili kuweza kujenga uwazi na kuleta imani katika zoezi zima la uhakiki wa malipo ya fidia.

Sisi wananchi na waathrika wa mradi huu tunashauri kuwa endapo zoezi la uhakiki litawahusisha watendaji wale wale waliohusika kufanikisha vitendo viovu vilivyotajwa hapo juu ni wazi kuwa wananchi hawatakuwa tayari kuwataja wote waliohusika na matendo haya. Hivyo fedha za serikali hazitaweza kuokolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, Halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Kinondoni hazitaweza kuwabaini watendaji wanojihusiha na vitendo vya rushwa na kukiuka taratibu za utendaji kazi katika masuala ya uboreshaji makazi yasiyopimwa.

Kutobainika kwa watendaji hawa wabovu kutapelekea vitendo vya aina hii kuendelea kushamiri katika masuala yanayohusu uboreshaji makazi yasiyopimwa na fedha nyingi sana za serikali kuendelea kupotea. Pia kutobainika kwa watendaji hawa wabovu ili waweze kuondolewa kutapelekea kuendelea kufedheheshwa kwa serikali mbele ya wananchi wake, ambao wanatazamia kupata huduma safi kutoka kwa watumishi wa serikali badala ya kuombwa rushwa, kupunjwa malipo ya fidia kutokana na kuwepo vitendo vya malipo hewa na baadhi ya watu kuzidishiwa malipo isivyo halali.


Ahsante
Majina sahihi zetu hapo chini


Waathrika wa Uhamishwaji Kimabavu Luguruni na Kibamba Hiospitali
(WUKILUKI)






Nakala

1) Mhe Jakaya M Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


2) Mhe Edward Lowassa
Waziri Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu


3) Mhe Mizengo Pinda
TAMISEMI


4) Taasisi ya Kuzuia Rushwa
Wilaya ya Kinondoni

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home