Tuesday, April 03, 2007

UDI yatambulishwa rasmi!

UDI YATAMBULISHWA RASMI
Programu ya UbungoTaarifa yaanza kutekelezwa

Hii ni taarifa rasmi kwa umma kuitambulisha Ubungo Development Initiative (UDI)- Asasi ya Maendeleo Ubungo. UDI ni asasi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa rasmi mwishoni mwa mwaka 2006. Dira ya UDI ni kuchangia katika kuleta maendeleo ya jimbo la Ubungo na maeneo jirani. UDI inatimiza wajibu huu kwa kuhamasisha uwajibikaji wa wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo. UDI inaweka mkazo zaidi katika uwezeshaji, ujasiriamali na elimu ya uraia.

Kwa kuanzia kwa mwaka huu wa 2007, UDI inatekeleza programu ya UbungoTaarifa. Hii ni programu inayohusisha kukusanya na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo. “ Tunatambua kwamba jimbo la Ubungo liko katika mkoa wa Dar es salaam ambao unafursa nyingi sana ambazo hajitumika bado. Yapo mashirika ambayo yanatoa msaada wa kisheria. Zipo taasisi zinazotoa mikopo. Na zipo taasisi mbalimbali ambazo zinafanya shughuli mahususi za kimaendeleo. Lakini wananchi waliowengi katika jimbo la Ubungo hawafahamu huduma zinazotolewa na taasisi hizi. Programu ya UbungoTaarifa inalenga kuwafahamisha uwepo wa huduma hizo. UDI itakuwa kiungo kati ya mashirika hayo na wananchi katika mwaka huu 2007”. Kuanzia mwaka 2008 na kuendelea UDI itazindua programu zingine za kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo ambayo kuna uhaba wa huduma.

Pia, UDI inapenda kuujulisha umma kwamba Taarifa yake ya Fedha kwa mwaka 2006 imeshafanyiwa ukaguzi wa mahesabu na wanachama na wananchi kwa ujumla wanaweza kuipitia. Aidha UDI inatumia fursa hii kutoa mwito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuweka wazi mapato na matumizi yao kama sehemu ya kuchochea uwajibikaji.

Wakati, huo huo- UDI inatoa mwito kwa watanzania kuwasaidia mitaji watanzania wenzao wasio na uwezo. “ kama kila mtanzania mwenye uwezo akimsaidia mtanzania mmoja tu mabadiliko ya hali ya juu yatatokea katika maisha ya watu wengi”. Hii imedhihirika kutokana na mfano wa Mama Halima Rashid ambaye ameomba kuambatana na UDI kutoa ushuhuda wake baada ya kusaidiwa na Kijana wa Kitanzania James Kitia aliyeko Ohio Marekani. Kijana huyu alisoma kwenye vyombo vya habari vya nyumbani kwa njia ya mtandao habari za Mama Halima ambaye alikimbiwa na mumewe baada ya kuwa na mtoto mwenye ulemavu na hivyo akakosa kabisa matunzo yake na ya mtoto. Baada ya kusoma habari yake James aliamua kumpatia mtaji kidogo wa shilingi laki mbili kupitia kwa mmoja wa waasisi wa Asasi ya Maendeleo Ubungo(UDI) Bwana John Mnyika. Bwana Mnyika alimkabidhi mchango tarehe 8 mwezi wa Machi, 2007 ambayo kwa bahati ilikuwa ni siku ya wanawake duniani. Leo ikiwa imepita takribani mwezi mmoja toka apatiwe mtaji huo ambao ameuelekeza katika biashara ya kuuza mayai kwa jumla na magazeti, Mama Halima yuko tayari kutoa ushuhuda wa mabadiliko ambayo mchango huo kidogo umeleta katika maisha yake.


Pia, UDI kama asasi inayosimamia uwajibikaji na maendeleo Ubungo na Tanzania kwa ujumla imefuatwa na kijana mkazi wa Jimbo la Ubungo katika kata ya Sinza Bwana Alistides Huntergration Buberwa ambaye amefungua kesi katika mahakama kuu kupinga Umri wa Kugombea Urais kuwa miaka 40 na fomu za Urais na Ubunge kutolewa gharama kubwa kuliko uwezo watanzania walio wengi hususani vijana. Katika kesi hiyo Alistides amepewa msaada wa Kisheria na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC). UDI kama asasi inayotoa sauti kwa wananchi katika masuala ya kimaendeleo imeamua kumpatia fursa hii aitambulishe kesi hiyo kwa umma.


Mwisho, UDI inaomba kuchukua fursa hii kuomba ushirikiano wa wananchi wa Ubungo, Serikali, Sekta binafsi na wadau mbalimbali wa kimaendeleo katika kutekeleza programu ya UbungoTaarifa na shughuli nyingine za kuhamasisha uwajibikaji na maendeleo katika jimbo Ubungo na maeneo jirani.


Wenu katika ujenzi wa TaifaHarold Makundi
Katibu Mtendaji
3/4/2007

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

Links to this post:

Create a Link

<< Home