Wednesday, May 28, 2008

Muktasari na Maazimio ya Semina ya Wakazi Kibamba

MUHTASARI NA MAAZIMIO YA SEMINA YA WAKAZI WA KATA YA KIBAMBA ENEO LA LUGURUNI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI KATI YAO NA SERIKALI KUHUSIANA NA MRADI WA MJI WA MFANO WA LUGURUNI.

TAREHE YA SEMINA : 24/05/2008
ENEO LA SEMINA: UWANJA WA MPIRA KIBAMBA ZAHANATI

UTANGULIZI:

Tatizo la msongamano wa magari na watu katikati ya jiji la Dar es Salaam halikuanza leo. Katikati ya miaka ya 90 hatua kadhaa zilianza kuchukuliwa na serikali ili kupunguza na hatimaye kuondoa tatizo hilo. Moja ya mikakati kabambe ilibuniwa na Tume ya Jiji iliyoundwa mahsusi kushughulikia matatizo ya utoaji huduma kwa wakazi wa jiji kutoka serikalini kwenda kwa wananchi. Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa Charles Keenja, ambaye sasa ni mbunge wa kuchaguliwa wa jimbo la Ubungo, lililo na kata 11, Kibamba ikiwemo, ilikuja na mbinu za kujenga barabara za pembezoni zikiunganisha votongoji kadhaa bila kupitia katikati ya jiji. Mpango huu ulionyesha mafanikio kwani msongamano ulidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, kufuatia sera ya biashara huria kukubaliwa nchini, idadi ya magari yaliyoingizwa nchini iliongezeka kwa kasi kubwa na hivyo kushinda ujenzi wa barabara hizo, na kulifanya tatizo kukua. Idadi ya watu nayo iliongezeka kwa kasi kubwa kufuatia hali duni ya huduma huko mikoani, na vijijini hivyo kuwafanya watu wengi kukimbilia jijini ili kujitafutia riziki na kuboresha maisha yao.

Serikali ilianza kujizatiti ili kukabiliana na msongamo wa watu na magari , kwa kuchukua hatua mbalimbali kama ya hivi karibuni ambapo aliyekuwa waziri mkuu, Mheshimiwa Edward Lowassa alibuni mpango wake wa kuruhusu magari kutofuata sheria za barabarani ili kupunguza msongamano. Mpango wake huu unajulikana kama Njia Tatu. Madhara kadhaa yakiwemo vifo kwa wananchi yametokea, na yanaendelea kutokea kufuatia utekelezaji huo wa amri ya Mheshimiwa Lowassa. Hadi sasa, serikali haijatoa msimamo wake rasmi kuhusu faida au hasara za mpango wa njia tatu, kama unakubalika kisheria na kama utaendelea kwa muda gani.

Serikali pia ilibuni mpango wa kujenga miji midogo yenye hadhi pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam ili kupunguza idadi ya watu wanaokwenda kufuata huduma katikati ya jiji. Moja ya mji huo wa mfano uliobuniwa na serikali ni Luguruni, uliopo kiasi cha kilometa 25 kutoka Dar es Salaam kuelekea Kibaha, mkoani Pwani. Eneo la Luguruni lipo ndani ya Kata ya Kibamba, Manispaa ya Kinondoni.Tathmini ya kwanza ilifanyika Juni mwaka jana.

Hata hivyo tangu serikali kuanza kuzilipa fidia familia 259 zinazohusika katika eneo hilo la mradi lenye ukubwa wa hekta 54, kumekuwepo na malalamiko mengi yaliyowahusisha watendaji wa serikali ya mtaa na kata ya Kibamba , manispaa ya Kinondoni na wizara ya Ardhi nyumba na makazi waliokuwa wasimamizi wa mradi huo. Tuhuma kadhaa za rushwa, uonevu, upendeleo na kutokuwajibika kwa viongozi hao ndiyo chanjo cha mgogoro huu.

MAHUDHURIO :

Katika semina hiyo iliyoitishwa na asasi ya kiraia ya Maendelo Ubungo( Ubungo Development Initiative,UDI) ikishirikiana na kikundi cha wananchi wa Kibamba Luguruni cha maendeleo na Uchumi(WAKILUKI) ilihudhuriwa na wananchi wapatao 125 kutoka maeneo mbalimbali ya kata ya Kibamba.Taarifa zisiso rasmi zilieleza kuwa baadhi wa wananchi walitishwa kuhudhuria kwamba polisi walikuwa wamejiandaa kuwakamata viongozi wa semina hiyo pamoja na wananchi watakaohudhuria kwani haikuwa na baraka za serikali, hivyo kuwa batili.

Kilichowasikitisha wananchi waliohudhuria semina hii ni kuona kuwa hakuna kiongozi wa wananchi hata mmoja aliyehudhuria wala kutoa udhuru wa kutokuhudhuria. Viongozi walioalikwa na ambao hakuna hata mmoja aliyehudhuria ni
1. Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kibamba
2. Afisa Mtendaji wa mtaa wa Kibamba
3. Afisa Mtendaji wa Kata ya Kibamba
4. Mheshimiwa Diwani wa kata ya Kibamba
5. Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Ubungo.
Viongozi hawa licha ya kupelekewa mialiko rasmi ya kuhudhuria semina hii muhimu ya wananchi ili wasaidie kujibu baadhi ya hoja za msingi, kuwaelekeza wananchi kwenye ufumbuzi wa tatizo hili na kujifunza kutoka kwa watoa mada waliamua kususia bila kutoa sababu zozote.

Pamoja na hali hiyo, wananchi waliohudhuria semina hiyo walikaa kwa utulivu na kuchangia katika kila mada kiasi cha kuifanya semina kuwa ya kufurahisha. Semina ilianza saa 4 asubuhi hadi saa 9 mchana.


MADA ZA SEMINA:
Mada muhimu zilizojadiliwa kwa pamoja kati ya waandaaji wa semina na wananchi ni pamoja na :
1. Ufafanuzi wa sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu namba 179.
2. Tangazo la serikali kuhusiana na masuala ya ardhi namba 78 la mwaka 2001
3. Mtiririko wa malipo halali ya fedha za serikali
4. Sera ya taifa ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi vifungu vya 4.9.1 hadi 4.9.3

Mada hizi zilijadiliwa kwa kina na kuchambuliwa kwa madhumuni ya kueleweka vizuri na wananchi wote. Wananchi wengi walikubali kuwa kuna upungufu mkubwa wa taarifa, sera, sheria na baadhi ya taratibu za serikali kutokueleweka kwao, na hicho ndicho kikwazo kikubwa na mbinu zinazofanywa na baadhi ya viongozi wabadhirifu kuwahadaa wananchi kwa kutokuzijuwa.

Baadhi ya vifungu muhimu vya sheria hii vilivyojadiliwa kwa kina ni pamoja na kile kinachoeleza bayana kuwa endapo serikali itaamua kuchukuwa eneo la mwananchi kwa ajili ya shughuli za kijamii, kwa manufaa ya umma, basi serikali italazimika kumshirikisha mmilikajiwa eneo hilo katika mchakato wa kufikia makubaliano ya fidia tangu mwanzo hadi mwisho, na kwamba malipo halali yaliyokubaliwa na wadau wote wawili yatafanyika mapema na kwa haki bila kumsababishia mwananchi huyo adha yoyote. Wananchi walisema kuwa kilichofanyika na serikali mkatika mradi huu ni tofauti na sheria zake yenyewe, kwamba hawakushirikishwa katika hatua yoyote ya tathmini hadi malipo, na ndiyo maana kuna malalamiko mengi. Waliongeza kuwa serikali iliwahadaa wananchi kwa kuwaambia kuwa watalipwa vizuri, bila kuwatajia njia watakazotumia kufikia kiasi cha malipo husika.

Katika uchambuzi wake mmoja wa watoa mada, Ndugu Chrisant Kibogoyo aliwaeleza wanasemina kuwa sheria ya fidia inatamka wazi kuwa :
• Fidia ni kwa bei ya soko la sasa
• Baadhi ya posho zinazoambatana na fidia ni
i) posho ya usumbufu
ii) posho ya makazi, ambayo ni bei ya kupanga nyumba kama inayolipiwa fidia katika eneo hilo
iii) posho ya usafiri wa mizigo kiasi cha tani 12 kwa kilometa 20
iv) posho ya upotevu wa faida iliyokuwa ikipatikana kutokana na mali inayolipiwa fidia.
• Utaratibu wa malipo ya fidia ya serikali unatumia fomu maalumu mbili, moja nyeupe na nyingine ya bluu. Hapa alifafanua kuwa kama kuna mwananchi aliyefanyiwa tathmini na kulipwa pesa bila kujaza na kusaini fomu hizo, basi malipo yale hayakutoka serikalini kwa kuwa serikali ni makini sana katika kufuata taratibu. Alidokeza kuwa kinachopangwa kufanyika sasa ni kuwahadaa wananchi wote waliolipwa kinyume na taratibu kukubali kuzijaza kinyemela ili kuhalalisha malipo hayo. Aliwatahadharisha wananchi kuwa macho na ujanja huo kwani kwa kufanya hivyo kutawafanya wapoteze haki zao. Kimsingi alisema kuwa inavyoonekana mradi huu wa mji wa mfano wa Luguruni labda siyo wa serikali bali wa wawekezaji fulani waliotumia mgongo wa serikali kuwaibia wananchi haki zao.Aliendelea kusema kuwa kwa jinsi anavyoifahamu serikali isingeweza kuwafanyia tathmini wananchi kwenye daftari( counter book) badala ya fomu maalumu ambazo serikali yenyewe ndiyo iliyozitengeneza ili zitumike nchi nzima kufanya tathmini.

Mtoa mada mwingine ambaye amesomea masuala ya uhasibu na ambaye amefanya kazi serikalini aliwaeleza wanasemina taratibu za malipo ya fedha za serikali kama ifuatavyo:

i)Chanzo cha madai kiwepo, kikiwa kimejazwa kwa usahihi( Proforma Invoice)
ii) Mtu wa kuanza mchakato wa malipo ya fedha za serikali atambulikane kwa jina na cheo chake
iii) Ukaguzi wa ofisa wa ngazi ya juu wa fomu ya chanzo cha madai ufanyike ili kujiridhisha kuwa fomu hiyo ni halali na imezajwa ipasavyo
v) Fomu hiyo iidhinishwe na ofisa mwingine anayetambulika na serikali kuwa yote yaliyomo ni sahihi kwa kadri ya uelewa wake
vi) Muandaaji wa malipo kwa hundi atie saini yake, muidhinishaji naye atie saini yake, na mlipaji pia atie saini yake.
vii) Malipo hayo yaambatanishwe na fomu inayoeleza sababu za malipo, fungu zilipotoka , jina na anuani ya mlipwaji na akaunti ya benki malipo yatakapotolewa.
viii) Kitabu maalumu cha kukabidhi hundi kitumike ( cheque register book) kikionesha jina la mlipwaji, kiasi cha malipo, namba ya cheki inayolipwa, na mlipwaji atie saini yake kuwa amepokea malipo.

Mtoa mada alisisitiza kuwa kama taratibu kama hizi hazikufuatwa wakati wa mchakato mzima wa kuandaa hadi kulipa fidia, basi kutakuwa na walakini katika malipo hayo. Aliongeza kuwa kimsingi, ni lazima kuwe na mkataba kati ya serikali na mlipwaji uliotiwa saini na wahusika wote wawili na kuthibitishwa na mwanasheria anayetabulika au hakimu anayefanya kazi serikalini, na kuwekwa muhuri . Hii ni hati ya kumbukumbu kwa kila mmoja wa walioingia mkataba ili pakitokea kutokuelewana baina yao warejee kwenye vifungu vya makubaliano yao.





MICHANGO KUTOKA KWA WANASEMINA:
• Pamoja na waziri Chiligati kusema kuwa tathmini itafanyika upya bado kuna tetesi kuwa viongozi wa mtaa wanawatumia wajumbe wa nyumba kumi kuwahadaa au kuwatisha wahusika kutokuhudhuria semina wala mikutano itakayoitishwa na watu wengine kuhusu mgogoro huu.
• Kwa wale waliolipwa tayari marekebisho yafanyike kulingana na sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 pamoja na fidia zote kulingana na bei ya soko.
• Mafunzo ya sheria , haki za binadamu na somo la uraia yafanike kila mtaa ili kuwaamsha wananchi wasiendelee kuminywa na viongozi wabadhirifu . Asasi za kiraia kama UDI na KIWALUKI ziwezeshwe kuendeleza mafunzo haya.
• Ubaguzi wa vyama vya siasa na dini vikemewe ili kuwaunganisha wananchi kwa ajili ya maendeleo yao. Baadhi ya viongozi wa CCM walio madarakani wanatumia suala la siasa kuwatenga wananchi ili wasielewe kinachoendelea.
• Viongozi waache kulindana kwa visingizo kuwa hakuna ushahidi wa kutosha. Malalamiko ya wananchi yakiwa mengi kwa kiongozi mmoja yatumike kama ushahidi wa kutoa madarakani
• Tathmini ya ardhi ya Kibamba izingatie bei ya soko la sasa ambapo kiwanja chenye ukubwa wa mita 20 kwa 20 kinauzwa kwa shilingi milioni 5.
• Wafanyakazi wote wa ardhi wakiwemo wa serikali ya mtaa na kata ya Kimbamba waliotuhumiwa na majina yao kukabidhiwa kwa Magufuli wasionekane kuhusiika na tathmini mpya kama itafanyika.
• Viongozi wa mtaa na kata waliokwepa kuhudhuria semina hii washinikizwe kuwaeleza wananchi sababu za kukataa kuhudhuria huku wakiwa ndiyo viongozi wanaotegemewa na wananchi.
• Viongozi wa kata na wilaya wanaoeneza uvumi kuwa Kibamba kuna kikundi cha kigaidi na wanasiasa uchwara watoe uthibitisho kwenye mkutano wa wananchi. Ilielezwa kuwa mnamo tarehe 8/ 5/2008 katika mtaa wa Kibwegere, mkuu wa wilaya ya Kinondoni Kanali Massawe alikwenda kuwahutubia wananchi wapatao 50 na kuwaambia kuwa:
i) Wananchi wa Luguruni na kwembe wamezuia mradi wa maendeleo wa Luguruni uliobuniwa na kufadhuiliwa na serikali
ii) Kuna kikundi cha wanasiasa uchwara na cha kigaidi cha KIWALUKI kinachohusika na kuwadanganya wananchi
iii) Kwamba kikundi hicho kilimsomea Mkuu wa Wilaya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi risala ya kutisha. Wananchi walisikitishwa na taarifa hizo potofu na kumtaka mkuu huyo awaombe radhi wananchi wa Kwembe na Luguruni kwa upotoshaji huo. Wao walisema kuwa hawajazuia mradi licha ya kutaka walipwe haki zao kulingana na sheria. Walisema kauli kama hizo za uongo zinazotolewa na viongozi wakuu wa Wilaya zinaonesha kuwa baadhi ya viongozi hawafanyi kazi kwa maslahi ya wananchi ila kwa kuwakumbatia viongozi wabovu na kuwadharau wananchi.Walegusia toleo la gazeti la Mtanzania la tarehe 30/4 2008 ambapo mkuu huyo wa wilaya alisemekana kumdanganya waziri kiasi cha mkuu wa mkoa wa Dar es salaam kumbana ili aseme ukweli. Walisema inaelekea mkuu huyo wa wilaya ana makusudi mengine na siyo kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Baada ya michango mingi kupokelewa kutoka kwa wanasemina na kujadiliwa, wote walikubalina na dhana ya kutoa maazimio ambayo waliomba yafikishwe kwenye vyombo vya habari na Bungeni kupitia kambi ya upinzani kwa kuwa mbunge wao wa CCM Mheshimiwa Charles Keenja amedhihirisha kuwa hawathamini wananchi wake, wala hataki kujihusisha na mgogoro huu kama vile hauhusu. Wameomba wabunge wa kambi ya upinzani wapeleke kilio chao bungeni ili wabunge wote kwa pamoja wapendekeze njia bora ya kumaliza mgogoro huu.


MAAZIMIO YA WANASEMINA

Sisi Wananchi wa kata ya Kibamba, hususan wakazi wa eneo la Luguruni, baada ya kuhudhuria semina hii na kujadiliana kwa kina baadhi ya matatizo yanayosababisha mgogoro kati yetu na serikali kuhusu malipo ya fidia tunaazimia kama ifuatavyo:-

i) Semina za namna hii zinazotoa mwanga wa elimu juu ya haki zetu na kutupatia fursa ya kutoa dukuduku zetu kwa uwazi na bila hofu ziendelee kutolewa na asasi za kiraia pamoja na serikali yetu .
ii) Elimu kwa umma kuhusu sera, kanuni na sheria mbalimbali za nchi yetu zisiishie kuwekwa kwenye makabati ya idara za serikali, badala yake zitawanywe kwa wananchi, asasi za kiraia na hata katika mtandao wa Intaneti ili wananchi wengi zaidi wanufaike nazo.
iii) Wakati wa semina kama hizi, wabunge wote wa Wilaya ya Kinondoni, bila kujali wanatokana na chama kipi cha siasa, wahudhurie ili panapotokea hoja za kisera na kisheria wazinukuu na kuzifanyia kazi huko bungeni kwa manufaa ya wananchi
iv) Katika mradi huu wa Luguruni kama wapo wawekezaji nje ya serikali wajitokeze ili wakutane na wananchi wanaohusika na kujadiliana jinsi ya kuendeleza mradi huu kwa pamoja, badala ya kujificha mgongoni mwa watendaji wachache wa serikali. Kama ni serikali yenyewe, basi itumie haki kuwalipa wananchi ili mradi uanze na kukamilika kwa wakati.
v) Hesabu kamili za wanaopaswa kulipwa fidia , waliokwisha kulipwa, na ambao hawajalipwa iwekwe wazi katika mbao za matangazo ili wananchi wazipitie , kuzikagua na kuwatambua waliolipwa isivyo halali.
vi) Pamoja na kuwalipa wahusika, serikali ifikiria upya uamuzi wake wa kumtaka kila aliyelipwa kubomoa nyumba yake kwani kuna baadhi ya majengo ambayo yakibakia yanaweza kutumika kama maghala ya kuhifadhi chakula, mizigo na kadhalika.matumizi bora ya fedha za umma yazingatiwe katika zoezi hili.
vii) Sheria zinazowalinda viongozi wa kuchaguliwa na wananchi wasiowajibika kuendelea kubakia madarakani hadi uchaguzi mwingine zifikiriwe upya, au kama kuna njia ya kuwaondoa viongozi hao zijulikane ili wananchi wazitumie kuwaadabisha.
viii) Demokrasia inaonekana kutokuwepo Kibamba. Tunaiomba serikali irudishe demokrasia Kata ya Kibamba ili wananchi wahudumiwe na viongozi badala ya viongozi kuwakandamiza wananchi.
ix) Miradi ya serikali isimamiwe na viongozi wa serikali badala ya wajumbe wa nyumba kumi ambao ni viongozi wa kisiasa. Wananchi watambulishwe kwa watendaji kabla ya kuanza kazi ili wawatathmini juu ya utendaji wao.
x) Viongozi waliokataa kuhudhuria semina watoe sababu mbela ya mkutano wa wananchi wote utakaoitisha karibuni.